Habari Magwiji!
Katika ulimwengu wa biashara, wazo lako lina nguvu pale tu unapoweza kuliwasilisha kwa wengine kwa ufasaha. Iwe unajaza fomu ya Entrepreneurship World Cup au unakutana na mwekezaji mtarajiwa kwenye mgahawa, unahitaji kitu kinachoitwa "Pitch."
Lakini "Pitch" ni nini hasa? Kwa mujibu wa mwongozo wa YALI Entrepreneurs, pitch ni wasilisho linalotumika kuelimisha wengine kuhusu kile ambacho biashara yako inalenga kutimiza, mara nyingi likiwa na lengo la kutengeneza ushirikiano au kupata uwekezaji.
Leo, Printiago inakuchambulia mwongozo wa YALI Entrepreneurs Workbook Three ili kukusaidia kutoa wazo lako kichwani na kuliingiza sokoni.'
1. Simulia Hadithi ya Ujasiriamali Wako
Hatua ya kwanza ya pitch kamilifu huanza kabla hata hujasimama mbele ya watu; huanza kwa kutathmini malengo yako na kuamua hadithi unayotaka kusimulia. YALI inakushauri ujibu maswali haya ya kigwiji:
Wewe ni nani? Eleza asili yako na nini kilikufanya uingie kwenye ujasiriamali.
Kwanini biashara yako ni ya kipekee? Jikite kwenye kile kinachokutofautisha na washindani wako.
Eleza shauku (passion) yako: Watu huvutiwa na mtu anayependa kile anachokifanya.
2. Changamoto ya Sekunde 30: "Elevator Pitch"
Hebu wazia unakutana na bilionea kwenye lifti na una sekunde 30 tu za kumuelezea biashara yako kabla lifti haijafika. Ungesema nini? Hiyo ndiyo inaitwa Elevator Pitch. Elevator pitch bora inapaswa:
- Kuwa wazi na fupi: Usizidi sentensi moja au mbili.
- Ionyeshe umuhimu: Eleza jinsi biashara yako inavyosaidia wengine.
- Iwe rahisi kukumbukwa: Inapaswa kumfanya msikilizaji aelewe kwanini unastahili kuungwa mkono.
3. Zungumza Kama Kiongozi (Public Speaking)
Maandishi mazuri bila wasilisho zuri ni kazi bure. Ili hadithi yako iguse mioyo ya watu, unapaswa kuzingatia mbinu za mawasiliano ya maneno na ya mwili:
|
Mawasiliano ya Maneno (Verbal) |
Mawasiliano ya Mwili (Nonverbal) |
|
Epuka maneno ya ziada: Acha kutumia maneno kama "e-h-h" au "yaani." Badala yake, nyamaza kidogo ili upate pumzi ya kuendelea. |
Simama wima: Posture nzuri huonyesha ujasiri. Simama wima ili sauti yako itokee kifuani na isikike vizuri. |
|
Badili toni ya sauti: Usiwe na sauti ya kuchosha! Ongea kwa msisimko na heshima kama unazungumza na rafiki wa karibu. |
Tumia mikono yako: Usikunje mikono. Tumia ishara za mikono kuwafanya wasikilizaji wajisikie wanakaribishwa kwenye hadithi yako. |
|
Sisitiza mambo muhimu: Ongea kwa taratibu na kwa shauku unapofikia sehemu muhimu ili kuacha alama kwa msikilizaji. |
Tazama watu machoni: Fanya wasilisho lako lionekane kama mazungumzo ya mtu na mtu kwa kutazama watu tofauti machoni kwa sekunde 4 hadi 5 kila mmoja. |
Kwanini Printiago ni Mshirika Wako?
Tunatambua kuwa miongozo mingi ya kimataifa kama hii ya YALI ipo katika lugha ya Kiingereza, jambo ambalo limekuwa kizuizi kwa wengi. Printiago ipo hapa kutafsiri mbinu hizi kwenda kwenye muktadha wa Kiswahili ili kuhakikisha kila mjasiriamali wa Kitanzania anakuwa tayari kunadi wazo lake kwenye majukwaa ya kimataifa kama GEC 2026.
0 comments