"Hata kama unauza maji ya kunywa barabarani au unalima nyanya, unahitaji 'Mfumo wa Biashara' (Business Model) ili usipoteze pesa zako bila kujua."
Utangulizi: Zaidi ya Biashara, Je! Una Mfumo?
Wajasiriamali wengi wadogo huanza biashara kwa kununua na kuuza tu. Lakini, mjasiriamali anayekua (Gwiji) anajua kuwa siri haipo kwenye bidhaa pekee, bali kwenye Mfumo wa Biashara (Business Model). Kwa mujibu wa Investopedia, Mfumo wa Biashara (Business Model) ni mpango wa biashara au kampuni wa jinsi ya kutengeneza faida. Inafafanua bidhaa unazouza, soko lako unalolenga, na gharama utakazotumia.
1. Mfumo wa Biashara (au Business Model kwa kimombo) ni nini hasa? (Kwa lugha yetu)
Fikiria mfumo wa biashara kama "Ramani ya Mchezo." Ni maelezo ya jinsi biashara yako inavyotengeneza thamani kwa wateja na jinsi inavyojilipa yenyewe.
Kwa mjasiriamali wa Tanzania, hii inaweza kuwa:
-
Thamani: Unatatua tatizo gani? (Mfano: Unauza bagia ambazo ni safi na zinafika ofisini kwa wakati).
-
Wateja: Ni akina nani? (Wafanyakazi wa maofisini Dar es Salaam wanaokosa muda wa kutoka kutafuta kifungua kinywa, au wakulima wa vijijini).
-
Gharama: Unatumia nini? (Mafuta, unga, mkaa, na usafiri).
2. Vipengele Muhimu vya Business Model
Ili ueleweke na wawekezaji (kama wale wa Sahara Sparks, Entrepreneurship World Cup (EWC), GoGettaz), lazima uwe na vitu hivi:
-
Thamani unayotoa (Value Proposition): Hiki ni kile kitu kinachomfanya mteja aache kununua kwa jirani na aje kwako. Labda ni bei nafuu, ubora, au urahisi.
-
Vyanzo Vya Mapato (Revenue Streams): Utapataje pesa? Je, ni kwa kuuza bidhaa moja kwa moja, au ni kwa mfumo wa "Subscribe" (kama unavyolipia ving'amuzi kila mwezi mfano vile vya AZAM, DSTV au NETFLIX)?
-
Mchanganuo wa gharama (Cost Structure): Je, utatumia pesa kiasi gani kutengeneza hicho unachouza?

3. Mifano Inayoishi Tanzania
-
Mfumo wa Uber/Bolt: Hawamiliki magari, lakini Mfumo wa Biashara (Business Model) wao ni kuunganisha wenye magari na abiria na kuchukua asilimia (commission).
-
Wauza Mitumba: Mfumo wa biashara wao ni kununua kwa jumla (gharama ndogo) na kuuza kwa rejareja (faida) baada ya kupambanua ubora (grade).
Kwa Nini Mjasiriamali "Mdogo na wa kati" Anahitaji Hii?
Bila Mfumo wa biashara (Business Model), utakuwa unafanya kazi kwa kubahatisha. Mfumo wa Biashara (Business Model) unakusaidia kujua kama biashara yako itadumu (sustainability). Kama unatumia shilingi 1,000 kutengeneza kitu na unauza 1,100, lakini gharama ya kukifikisha kwa mteja ni 200, huo mfumo wa biashara (Business Model) umefeli (unapata hasara ya 100).
Chanzo: Investopedia (Tafsiri ya Mfumo wa Biashara)
1 comment
Tafakari ya Kigwiji #01
Mzee wangu, biashara nyingi nchini kwetu hazifi kwa sababu ya kukosa mtaji, bali zinafia kwenye Business Model mbovu. Unaweza kuwa na bagia tamu kuliko zote mjini (bidhaa nzuri), lakini kama huna mfumo wa kuzifikisha kwa watu (logistics) au bei yako hailingani na gharama za mafuta ya kula, utafilisika.
Kabla ya kuanza “Kusink bucket” lako, chukua karatasi na uandike: “Nitapataje pesa? Nitatumia kiasi gani? Na kwa nini watu wanunue kwangu?” Ukijibu hayo, wewe ni Gwijji tayari!